Hii leo, Melania Trump aliungana na Rais Donald J. Trump kuwakaribisha Rais Uhuru Kenyatta wa Jamhuri ya Kenya na Mkewe, Margaret Kenyatta kwenye Ikulu.
Bi. Trump na Bi. Kenyatta walikuwa pamoja wakati wa adhuhuri wakifanya mazungumzo wazi yaliyoangazia malengo yao ya pamoja na miradi ya kila mmoja wao kwa niaba ya watoto. Kampeni ya Bi. Trump inayoitwa Be Best na ile ya Bi. Kenyatta iitwayo Beyond Zero Initiative imeungana chini ya lengo la kuboresha na kulinda ustawi wa watoto.
Bi. Trump anapanga kutembelea Afrika mnamo Oktoba, ili kuimarisha zaidi ushirikiano wa ndani na wa muda mrefu uliopo kati ya Marekani na nchi nyingi za Afrika.
“Jitihada ambazo Kenya inafanya ili kuboresha maisha ya watoto wake ni ambazo Marekani inathamini pia,” asema Mkewe Rais, Melania Trump. “Nina hamu kubwa sana ya kutembelea bara la Afrika. Asante Margaret Kenyatta, kwa kuja kwenye Ikulu hii leo. Ninatazamia fursa zijazo za sisi kushirikiana.”