rss

Taarifa ya Pamoja kutoka kwa Rais Donald J. Trump na Rais Uhuru Kenyatta

English English, Français Français

Ikulu Ya Rais Wa Marekani
Ofisi ya Katibu wa Uhusiano Mwema na Vyombo vya Habari
Ya Kutolewa Kwa Vyombo Vya Habari Mara Moja
27 Agosti, 2018

 

Rais Donald J. Trump alimkaribisha Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwenye Ikulu hii leo. Ili kuadhimisha miaka 55 ya uhusiano mwema kati ya Marekani na Kenya, na kwa kutambua kupanuka kwa upeo na kina cha ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, viongozi hao waliamua kuuinua uhusiano huo kuwa Ushirikiano wa Kimkakati, na kuuthibitisha kama nguzo ya amani, uthabiti na uongozi mwema barani Afrika na katika kanda ya Bahari ya Hindi. Ushirikiano huu wa Kimkakati baina ya Marekani na Kenya utajumuisha mazungumzo ya kila mwaka ili kuendeleza mafanikio ya pamoja.

Rais Trump alivipongeza Vikosi vya Ulinzi vya Kenya kwa huduma zao na kujitolea kwao katika kupigana na al-Shabaab na ISIS nchini Somalia. Rais Trump pia aliipongeza Kenya kwa kuwa mstari wa mbele katika vita dhidi ya ugaidi na kwa kuzidi kujitolea katika juhudi hizi. Viongozi hao walithibitisha upya na kuimarisha kujitolea kwao kuendelea kushirikiana kupambana na magaidi wenye misimamo mikali inayoleta vurugu na ambao husababisha watu wasio na hatia kupoteza Maisha na kunyimwa haki msingi za kibinadamu. Ili kuimarisha zaidi ushirikiano huu wa kupambana na ugaidi, Rais Trump aliukaribisha uamuzi wa Kenya kujiunga na Ushirikiano wa Kimataifa wa Kushinda ISIS (Global Coalition to Defeat ISIS).  Rais Trump pia alimpongeza Rais Kenyatta kwa juhudi zake za kidiplomasia za kuleta amani nchini Sudani Kusini na kwa eneo nzima kwa ujumla.

Viongozi hao waliahidi kuzidisha ushirikiano wao katika masuala ya ulinzi na usalama, kufuatia ununuzi wa vifaa vya kijeshi vilivyotengenezewa Marekani na kuapa kuimarisha uwezo wa Vikosi vya Ulinzi vya Kenya. Aidha, Marekani iliahidi kuimarisha uwezo wa Kenya wa kushughulikia majanga na hali za hatari za kitaifa.

Rais Kenyatta alimshukuru Rais Trump kwa usaidizi unaozidi kutolewa na Marekani katika juhudi za utawala wa Kenyatta kuleta uwajibikaji zaidi, uwazi, na kujenga taasisi. Kama demokrasia zizingatiazo utaratibu wa kanuni za kimataifa,  Marekani na Kenya zina maono ya pamoja ya kuwepo na jamii wazi na huru. Hii ni pamoja na uhuru wa kimataifa wa kusafiri, hasa katika eneo la Bahari za Hindi na Pacific.

Viongozi hao waliahidi kupanua ushirikiano wao wa kiuchumi wenye lengo la kuimarisha mataifa yao na kuleta mafanikio zaidi ya wananchi wake. Kwa hili, Rais Trump alimshukuru Rais Kenyatta kwa kuukaribisha ujumbe wa Marekani wa Baraza la Ushauri kuhusu Kufanya Biashara Barani Afrika. Ili kuimarisha zaidi ushirikiano wao wa kiuchumi, viongozi hao wawili walikubali kubuni Jopo Kazi la Biashara na Uwekezaji la Marekani na Kenya ili kuangazia mbinu za kupanua zaidi uhusiano kati ya nchi hizi mbili. Aidha Rais hao wana furaha kutangaza kuwa serikali zao zimeanzisha safari za ndege za moja kwa moja kutoka Nairobi hadi Jiji la New York, hatua ambayo itaimarisha uhusiano wa kiuchumi na kitamaduni kati ya nchi hizi mbili kuu.

Huku wakitambua umuhimu wa miundombinu ya hali ya juu, Rais Trump na Rais Kenyatta walikaribisha pendekezo la shirika la uhandisi na ujenzi la Kimarekani, Bechtel Corporation, kujenga barabara kuu ya kisasa ya kutoka Nairobi hadi Mombasa. Pande zote mbili zilikubali kushauriana zaidi ili kukamilisha masharti ya mkataba wa ufadhili.

Mkataba huu, na mikataba mingine na ushirikiano zaidi wa kibiashara wenye thamani ya takriban milioni $900 dola za Marekani iliyotangazwa wakati wa ziara hiyo inatarajiwa kuleta maelfu ya nafasi za kazi kwa Marekani na Kenya, hivyo kuimarisha zaidi mafanikio na ushindani wa kiuchumi wa nchi zote mbili.


Tafsiri hii hutolewa kwa hisani tu hivyo chanzo chake asili katika lugha ya Kiingereza ndicho pekee kinapaswa kuonwa kuwa chanzo kikuu.
Taarifa kwa Barua pepe
Ili kujisajili kwa taarifa au kufikia mapendekezo yako ya mteja, tafadhali ingiza maelezo yako ya mawasiliano hapa chini.